Neno jitambue
ni kubwa na lenye kubeba maana nyingi kwa mtu yeyote anayekutana nalo, jitambue
ni hali ya mtu kujifahamu yeye ni nani na anatakiwa afanye nini katika kila
eneo la maisha yake.
Kuna watu
wanatembea lakini ukiwaangalia wamekata tamaa, wamezingirwa na mawazo lukuki
yanayowafanya wasiwe na mawazo mapya katika fikra zao. Wamegubikwa na mambo mengi kiasi cha kujiona
kwa nini wanaishi katika ulunwengu huu.
Watu wengi wamekuwa wepesi
sana kukimbilia kwa rafiki zao ili kuomba msaada wa mawazo ya nini wafanye kwenye maisha na hasa wakati wa shida. Imani iliyojengeka kwa wengi katika jamii
yetu ni kuwa, ushauri ni kitu muhimu sana kwa kila hatua.
Unaamka
umenuna, unaoga umenuna, unavaa umenuna, unakwenda kazini umenuna. Jioni
unarudi umenuna! Inasaidia nini? Kama una dukuduku na mke au mumeo, mwambie.
Zungumza naye. Unanuna nini? Haitakusaidia kitu. Njia njema zaidi ya kumaliza
matatizo ndani ya nyumba ni mazungumzo. Chukua hili kutoka kwangu.
Hakuna kitu
kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja la chini na mtu wa
kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna madhara makubwa.
Ni imani
yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu
tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi
mbele ya wenzetu.
Watu wengi
wamenifuata na kuniambia kuwa hawana furaha ya maisha. Niliwauliza kwa nini
hawana furaha? Bila kusita kila mtu aliniorodheshea wingi wa shida zinazomkabili
ambazo kwa namna moja au nyingine zimemfanya akose raha.
Lakini, je,
kuwa na shida au mahitaji ya fedha ya matumizi, kuachwa na mume au kufiwa ni
lazima iwe sababu ya mtu kukosa furaha? Mbona kuna wengine wanafurahia ujane
kwa sababu tu wamebaki na mali za urithi?
Siku zote kikwazo cha furaha ya
mwanadamu ni watu ingawa mazingira nayo huchangia kwa kiasi fulani lakini
binadamu wenzake ndiyo adui namba moja wa raha ya mtu.
Tunaweza kujiuliza kwa nini watu ni
tatizo? Jibu ni ni jepesi, mwanadamu hawezi kujihukumu kama hakuhukumiwa na
wenzake. Katika hali ya kawaida, ukosefu wa furaha husababishwa na hukumu za
watu ambazo huleta mawazo yanayoweza kumfanya mtu ajione duni.
Kitaalamu, ile hali ya kujiona mtu
wa hali ya chini, uliyeshindwa kufanikiwa katika hili, uliyepitwa na wenzako
kwa uwezo fulani, ndiyo huleta hali ya kukosa raha. Hii ina maana kuwa kukosa chakula
chenye chumvi nyikani kusikokuwa na watu hakuwezi kukukosesha furaha kwa namna
yoyote kama tu mawazo yako yanautetea udhaifu wako.
Tabia kuu ya mwanadamu ni ulinganifu
na wenzake, kile ambacho anaamini hajakipata ila mwenzake anacho ndicho huwa
kikwazo cha furaha yake. Hii ina maana
kwamba tabia ya mtu kuwaza jinsi binadamu wenzake wanavyomfikiria ndiyo kisa
ambacho humuondolea furaha.
Wakati wote tabia ya watu wasiokuwa
na furaha huwa ni kufikiri namna ambavyo wenzake wanamfikiria. “Nimeshindwa
kuendeleza duka langu, wenzagu si watanicheka?” Mawazo ya namna hii ya kuona
wewe ni sehemu ya wale ndiyo mfereji wa kupoteza furaha yako.
Kwa kawaida, binadamu anapojifikiri
mwenyewe bila kujilinganisha na wenzake hukubaliana na udhaifu wake na hilo
haliwezi kuwa chanzo cha yeye kupoteza furaha yake.
Adamu na Hawa, wazazi wa kwanza wa
binadamu kwa mujibu wa kitabu cha Biblia, hawakuuona udhaifu wao walipokuwa
wakijifikiria wenyewe na nafsi zao mpaka nyoka alipowaletea mawazo ya kuazima
kutoka kwa mtu mwingine ambayo yaliwageuza na kujiona wanyonge, wakatamani kuwa
kama mtu.
Inaelezwa kwenye kitabu hicho kuwa,
nyoka aliwauliza kama wanakubaliana na katazo la kutokula tunda la mti wa uzima
ambapo wao walisema NDIYO, lakini waliporithishwa mawazo kuwa kuna mwingine
anayewazidi ufahamu, waligeuka na kujiona wanyonge, wasiokuwa na utimilifu,
wakosefu wa furaha na hivyo kuamua kula tunda si kwa sababu walipenda bali
walitamani kufanana na mtu mwingine.
Ushauri wangu: Kama mtu anataka kuwa
na furaha ya maisha anatakiwa kujifikiria zaidi mwenyewe na kuepukana na tabia
za kukopa utu wa mwingine na kutamani kufanana naye. Mtu unaweza kuugua kwa
muda, ukitulia utapona, unaweza kuwa maskini, lakini ukiacha kukata tamaa na
kuongeza bidii utatajirika, hayo ndiyo maisha.
Kukosekana kwa jambo fulani
unalolihitaji leo haina maana utu wako umepungua bali ni mapito ya maisha
ambayo unatakiwa kukabiliana nayo wewe mwenyewe na mawazo yako na kuzishinda
changamoto zote.
Kama ni mawazo ya kuazima basi
lazima yawe yale ya kukusaidia mbinu za kushinda na si yatakayokufanya kujiona
dhaifu mbele ya binadamu wenzako. Jipe moyo ushindi wa hayo yanayokukosesha
furaha upo mikononi na akilini mwako.
Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu
timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima
tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Kitaalamu, hakuna jambo ambalo
hutokea maishani bila sababu maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako au kwetu
ndani ya jamii tunayoishi kunatokana na jinsi tunavyoenenda.
Watu waliopitia matatizo na shida
duniani wameorodhesha mambo mengi
yaliyowafanya wawe kama walivyo, walipitia shida, walifeli, walishindwa na
baadae wakajitambua na kuinuka na kuanza upya haujachelewa simama na anza tena
utashangaa na kuwa ushuhuda kwa watu wengine.
Watu wengi wanayaona mafanikio kwa
watu weupe tu hapana, hata wewe unaweza kufanikiwa ukijitambua na ukiishi
katika mtazamo wako na wala sio mtazamo wa mtu mwingine kwani kila mtu ana wazo
lake na ana kipawa chake alichojaaliwa na Mungu na ndio maana unaweza kuiga mtu
kuuza vitumbua kumbe sio karama yako kesho yake unaacha kwa kukosa uvumilivu wa
kuungua na moto na harufu ya mafuta.
Simama katika nafasi yako na amua kuishi kwa
jinsi unavyotaka wewe huku ukiwa na malengo yenye dhima ya kufikia ushindi wa
hali ya juu sana.
Hakuna kinachotokea kwenye maisha
yako bila kuwa na sababu, umezaliwa ili upambane na kufikia kilele cha hatima
yako na siku zako za kuishi anajua yeye aliyekuleta hapa duniani. Na mwisho wa siku zitatakiwa hesabu
zake. Utaulizwa ulifanya nini kule
ulikokwenda yaani hapa duniani.
Ebu yaangalie haya hapa chini na kuyafanyia
kazi kama unataka kujitambua na kuwa mahali pa kuheshimika katika jamii
inayokuzunguka:-
MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi
unavyoonekana. Muonekano ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa
ujumla. Hata siku moja hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata
kama ana kipaji kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili
huchangia mtu kudharauliwa katika jamii anayoishi. Linaweza kuwa jambo dogo
sana lakini ni moja kati ya sababu kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani
yako mbele ya wenzako.
Mazungumzo
Hapa naomba nieleweke kuwa
unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli
zisizo na busara zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na
mantiki huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi.
Biblia inasema penye wingi wa maneno hapakosi uovu.
UTENDAKAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote heshima ya
mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku wengine
wakijiendekeza kwa tabia ya kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchangia
kubomoa heshima yako mbele ya jamii. Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.
KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za kuahidi mambo
halafu unashindwa kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza
heshima yako katika jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na
kutotimiza.
SIFA ZISIZO NA MAANA
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa
mwandishi mwandamizi aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha, marehemu Adolf
Balingilaki, ambao unasema kwamba:
“Ukitafuta heshima kwa gharama ya
juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha nini? Siku
zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya
kujiinua, watu watakudharau.
KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala la uaminifu ni pana, kuna
uaminifu wa fedha, siri, dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema kila
unachoaminiwa lazima ukitunze kwani ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa
utashusha heshima yako.
Karibu
tuelimishane na kusaidia pale unapojua niko tayari kujifunza toka kwako;
naamini ili niweze kujua zaidi natakiwa kujifunza kupitia wenzangu.
Karibuni
sana tusonge mbele kwa ushindi.
Lusako
Mwakiluma
No comments:
Post a Comment