Friday, March 7, 2014

WANAWAKE TUJITOE KUWASAIDIA WENGINE




Leo tarehe 8/3/2014 ni siku ya wanawake Duniani, wanawake wenzangu napenda kuwatakia siku njema na kuwatia nguvu kwa kuwapa hongera kila mwanamke kwa kuhadhimisha siku ya wanawake duniani kote: 

Napenda kuwaomba wanawake wenzangu tusiridhike na mafanikio madogo tuliyonayo: Ebu tujitoe kwa kazi za kujitolea katika jamii yetu ili kuweza kuwasaidia wanawake wenzetu wenye hali duni kuhakikisha wanapata nguvu za kuweza kusimama kwa kuwafundisha mbinu za kufanikiwa na kuinua hali zao hasa wasiokuwa nacho, wasiojiweza, walemavu na wajane na waishio katika hali ngumu.  Tusome kwa bidii kwa wale wasomi, na wale wajasiriamali wasimame katika sehemu zao kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya hali ya juu ili tukimbizane na soko la Kimataifa.

Wanawake wenye elimu tuzitumie elimu zetu kuwasaidia wasio kuwa na elimu kwa kuwafundisha jinsi ya kuwaelimisha wenzao, na pia kuwajengea misingi imara mabinti zetu walioko vyuoni na mashuleni  kwa kuanzia elimu ya awali kwa kuwashuhudia yale tuliyopitia sisi, ili kuwa chachu katika maisha yao ya leo na hata siku za usoni.  Changamoto na fursa tulizozipata kama wanawake wenye mwamko na mafanikio.

Utandawazi usiwe kigezo cha wao kuchukulia maisha kwa njia ya mkato tuwaelekeze kwamba wajitume sana na kufanya kazi kwa bidii popote walipo iwe mashuleni, majumbani, makazini na hata katika kazi za kujitolea. 

 Kwani unapotoa ndipo pale unapopokea wakitambua asiye fanya kazi na asile.

Tuwajengee uwezo  wa malezi; wazazi na walezi ili kuwanusuru  watoto na wasichana  kubakwa na  ndoa za umri mdogo zipigwe vita.
Kuwaelimisha wasichana na kuwapa fursa  wenyewe kutoa mawazo yao kuhusu udhalilishaji wa kijinsia mfano: Wale waliodhalilishwa na wale wanaotishiwa kudhalilishwa,  kutoa mbinu kwa wale ambao hawajakutana na hali hizo ili wajue mbinu za wadhalishaji na kujinusuru, na kutokuwa tayari kupokea zawadi ndogondogo zenye kuleta madhara.
Kuhakikisha wasichana na mabinti zetu  wanapata elimu ya kujitambua na kujithamini ili waweze kutimiza ndoto zao wasikwame njiani kwa majuto.

Kuhakikisha wimbi la ukeketaji linakwisha kabisa kwa kuwapa elimu wanaume kutosumbukia mabinti waliokeketwa na kuwapa mabinti hasara za ukeketaji.

Kuhakikisha tunawajengea uwezo makahaba na wanaofanya biashara haramu ya ngono kuwapatia elimu na mitaji ili waweze kujiajiri au kuachana kabisa na dhana ya ngono zembe kwa  kuuza mwili kwa faida ya pesa kidogo, yaani pesa ya kula leo tu. “Tuwafundishe kuvua samaki na sio kuwapa samaki wale na kesho wakaomba tena”.

Kuhakikisha wazazi na walezi wanapata stadi  za malezi yenye kuzingatia utandawazi bila kuharibu mila na desturi zetu tulizopitia sisi kwani ukimuelimisha mtoto wa kike umelielimisha Taifa kwa ujumla.  Watoto wasikurupuke kwa kuiga kwani kupitia kuiga ndio wanauandaa mwisho wao,  wanatakiwa wawe wabunifu wa vipaji vya wenyewe.

Changamoto wanazopitia wanawake wenzetu
Katika kuadhimisha siku hii tulikuwa pia tunaiomba serikali na wadau iwaangalie wanawake wenzetu wa kimasai, kisukuma na kikurya wanaopitia hali ngumu katika kufanya kazi kwa bidii kwa kuchunga kwa umbali mrefu, kutafuta kuni umbali mrefu, kupika, kufua, kuangalia watoto na  mwisho wa siku walaji ni wakinababa yaani wanaume kwa kudhalilishwa, kunyanyaswa na hata kukosa amani ndani ya nyumba zao wenyewe.
Wapewe msaada wa elimu endelevu ili na wao waweze kusimama katika jamii wakiwa wanawake wenye maamuzi ndani ya nyumba zao na pia wapatiwe elimu wenza wao yaani wanaume na kuelewa mwanamke ni mtu muhimu sana katika jamii yetu na kumpa nafasi ya kutoa maamuzi ndani ya nyumba zao na kusikilizwa na kupewa kipaumbele pale inapotakiwa kufanya hivyo.

Naamini kupitia siku hii wanawake wenzangu mtakuwa mmeamka kwenye blanketi zito la usingizi na kuanza kupiga hatua ili tuweze kuwa wasaidizi bora na sio bora wasaidizi.  Kwani katika kila mwanaume aliyefanikiwa yuko mwanamke nyuma yake.  Tuige mifano ya wamama kama Mama Obama, Dada yetu Oprah Winfrey, Mama Salma Kikwete na Mama Pinda tusimame daima kuhakikisha wanawake wanafanikiwa katika kila Nyanja Kiuchumi, kijamii, Kisiasa na Kielimu kwa kuelimishana na kufundishana kwa upendo na ukarimu tukijifunza kutoka kwa waliofanikiwa.

Mungu ibariki Tanzania, wabariki wanawake wote!!!!

Naomba tuamini kwa pamoja tunaweza.

Na: Bi Lusako Mwakiluma


No comments:

Post a Comment