Wednesday, August 20, 2014

MTAZAMO UNABADILISHA KILA KITU



 Mpendwa msomaji wa mada zangu napenda nikwambie kitu, mtazamo ni kila kitu, unaweza ukatazama ng’ombe ukamuona simba kwa jinsi unavyoona wewe ndivyo unavyotengeneza kuhamisha kitu katika fikra zako, anza leo hii kutazama kwa jicho la ndani.


Ebu ona ushindi na baki ukifikiria ushindi wa hali ya juu, simamia mtazamo na uone jinsi unavyoweza kubadilisha maisha yako kwa haraka zaidi.  Kwani fikra ndio kila kitu ulizoea kuwaza mabaya leo hii unaanza kufikiria mazuri  na utaona uzuri ukikusogelea.


Angalia waliofanikiwa, waulize walipitia wapi na nini mpaka wakafikia hapo,  tazama kwa jicho la tofauti yaani jicho la ndani yako tokea moyoni mwako huku ukiwa na shauku ya mabadiliko ya hali ya juu.


Ongea na moyo wako, ongea na kioo chako, ongea ndani ya gari yako, ongea katika chumba chako cha siri utaona jinsi mabadiliko yanavyoenda kutokea kwa kupata shauku nzuri ya kukubadilisha na kuwa mtu mpya na wa tofauti kwa kuwaza chanya kila siku katika jamii na maisha yako kwa ujumla.

Karibu tuendelee kutiana moyo, kuinuana kila wakati.

Na: Lusako Mwakiluma

Monday, August 4, 2014

JITAMBUE ILI UFANYE ULIYOKUSUDIA KUYAFANYA

 Neno jitambue ni kubwa na lenye kubeba maana nyingi kwa mtu yeyote anayekutana nalo, jitambue ni hali ya mtu kujifahamu yeye ni nani na anatakiwa afanye nini katika kila eneo la maisha yake.  

Kuna watu wanatembea lakini ukiwaangalia wamekata tamaa, wamezingirwa na mawazo lukuki yanayowafanya wasiwe na mawazo mapya katika fikra zao. Wamegubikwa na mambo mengi kiasi cha kujiona kwa nini wanaishi katika ulunwengu huu.

Watu wengi wamekuwa wepesi sana kukimbilia kwa rafiki zao ili kuomba msaada wa mawazo ya nini wafanye  kwenye maisha na hasa wakati wa shida.  Imani iliyojengeka kwa wengi katika jamii yetu ni kuwa, ushauri ni kitu muhimu sana kwa kila hatua.

Unaamka umenuna, unaoga umenuna, unavaa umenuna, unakwenda kazini umenuna. Jioni unarudi umenuna! Inasaidia nini? Kama una dukuduku na mke au mumeo, mwambie. Zungumza naye. Unanuna nini? Haitakusaidia kitu. Njia njema zaidi ya kumaliza matatizo ndani ya nyumba ni mazungumzo. Chukua hili kutoka kwangu.  

Hakuna kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja la chini na mtu wa kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna madhara makubwa.

Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.

Watu wengi wamenifuata na kuniambia kuwa hawana furaha ya maisha. Niliwauliza kwa nini hawana furaha? Bila kusita kila mtu aliniorodheshea wingi wa shida zinazomkabili ambazo kwa namna moja au nyingine zimemfanya akose raha.

Lakini, je, kuwa na shida au mahitaji ya fedha ya matumizi, kuachwa na mume au kufiwa ni lazima iwe sababu ya mtu kukosa furaha? Mbona kuna wengine wanafurahia ujane kwa sababu tu wamebaki na mali za urithi?

Siku zote kikwazo cha furaha ya mwanadamu ni watu ingawa mazingira nayo huchangia kwa kiasi fulani lakini binadamu wenzake ndiyo adui namba moja wa raha ya mtu.

Tunaweza kujiuliza kwa nini watu ni tatizo? Jibu ni ni jepesi, mwanadamu hawezi kujihukumu kama hakuhukumiwa na wenzake. Katika hali ya kawaida, ukosefu wa furaha husababishwa na hukumu za watu ambazo huleta mawazo yanayoweza kumfanya mtu ajione duni.

Kitaalamu, ile hali ya kujiona mtu wa hali ya chini, uliyeshindwa kufanikiwa katika hili, uliyepitwa na wenzako kwa uwezo fulani, ndiyo huleta hali ya kukosa raha. Hii ina maana kuwa kukosa chakula chenye chumvi nyikani kusikokuwa na watu hakuwezi kukukosesha furaha kwa namna yoyote kama tu mawazo yako yanautetea udhaifu wako. 

Tabia kuu ya mwanadamu ni ulinganifu na wenzake, kile ambacho anaamini hajakipata ila mwenzake anacho ndicho huwa kikwazo cha furaha yake.  Hii ina maana kwamba tabia ya mtu kuwaza jinsi binadamu wenzake wanavyomfikiria ndiyo kisa ambacho humuondolea furaha.

Wakati wote tabia ya watu wasiokuwa na furaha huwa ni kufikiri namna ambavyo wenzake wanamfikiria. “Nimeshindwa kuendeleza duka langu, wenzagu si watanicheka?” Mawazo ya namna hii ya kuona wewe ni sehemu ya wale ndiyo mfereji wa kupoteza furaha yako.

Kwa kawaida, binadamu anapojifikiri mwenyewe bila kujilinganisha na wenzake hukubaliana na udhaifu wake na hilo haliwezi kuwa chanzo cha yeye kupoteza furaha yake.

Adamu na Hawa, wazazi wa kwanza wa binadamu kwa mujibu wa kitabu cha Biblia, hawakuuona udhaifu wao walipokuwa wakijifikiria wenyewe na nafsi zao mpaka nyoka alipowaletea mawazo ya kuazima kutoka kwa mtu mwingine ambayo yaliwageuza na kujiona wanyonge, wakatamani kuwa kama mtu.

Inaelezwa kwenye kitabu hicho kuwa, nyoka aliwauliza kama wanakubaliana na katazo la kutokula tunda la mti wa uzima ambapo wao walisema NDIYO, lakini waliporithishwa mawazo kuwa kuna mwingine anayewazidi ufahamu, waligeuka na kujiona wanyonge, wasiokuwa na utimilifu, wakosefu wa furaha na hivyo kuamua kula tunda si kwa sababu walipenda bali walitamani kufanana na mtu mwingine.

Ushauri wangu: Kama mtu anataka kuwa na furaha ya maisha anatakiwa kujifikiria zaidi mwenyewe na kuepukana na tabia za kukopa utu wa mwingine na kutamani kufanana naye. Mtu unaweza kuugua kwa muda, ukitulia utapona, unaweza kuwa maskini, lakini ukiacha kukata tamaa na kuongeza bidii utatajirika, hayo ndiyo maisha.

Kukosekana kwa jambo fulani unalolihitaji leo haina maana utu wako umepungua bali ni mapito ya maisha ambayo unatakiwa kukabiliana nayo wewe mwenyewe na mawazo yako na kuzishinda changamoto zote.

Kama ni mawazo ya kuazima basi lazima yawe yale ya kukusaidia mbinu za kushinda na si yatakayokufanya kujiona dhaifu mbele ya binadamu wenzako. Jipe moyo ushindi wa hayo yanayokukosesha furaha upo mikononi na akilini mwako.

Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.

Kitaalamu, hakuna jambo ambalo hutokea maishani bila sababu maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako au kwetu ndani ya jamii tunayoishi kunatokana na jinsi tunavyoenenda.

Watu waliopitia matatizo na shida duniani wameorodhesha  mambo mengi yaliyowafanya wawe kama walivyo, walipitia shida, walifeli, walishindwa na baadae wakajitambua na kuinuka na kuanza upya haujachelewa simama na anza tena utashangaa na kuwa ushuhuda kwa watu wengine. 

Watu wengi wanayaona mafanikio kwa watu weupe tu hapana, hata wewe unaweza kufanikiwa ukijitambua na ukiishi katika mtazamo wako na wala sio mtazamo wa mtu mwingine kwani kila mtu ana wazo lake na ana kipawa chake alichojaaliwa na Mungu na ndio maana unaweza kuiga mtu kuuza vitumbua kumbe sio karama yako kesho yake unaacha kwa kukosa uvumilivu wa kuungua na moto na harufu ya mafuta.

Simama katika nafasi yako na amua kuishi kwa jinsi unavyotaka wewe huku ukiwa na malengo yenye dhima ya kufikia ushindi wa hali ya juu sana.

Hakuna kinachotokea kwenye maisha yako bila kuwa na sababu, umezaliwa ili upambane na kufikia kilele cha hatima yako na siku zako za kuishi anajua yeye aliyekuleta hapa duniani.  Na mwisho wa siku zitatakiwa hesabu zake. Utaulizwa ulifanya nini kule ulikokwenda yaani hapa duniani.

 Ebu yaangalie haya hapa chini na kuyafanyia kazi kama unataka kujitambua na kuwa mahali pa kuheshimika katika jamii inayokuzunguka:-

MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi unavyoonekana. Muonekano ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku moja hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana kipaji kikubwa kiasi gani.

Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili huchangia mtu kudharauliwa katika jamii anayoishi. Linaweza kuwa jambo dogo sana lakini ni moja kati ya sababu kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani yako mbele ya wenzako.

Mazungumzo
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi. Biblia inasema penye wingi wa maneno hapakosi uovu.

UTENDAKAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza kwa tabia ya kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchangia kubomoa heshima yako mbele ya jamii. Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.

KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza heshima yako katika jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na kutotimiza.

SIFA ZISIZO NA MAANA
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa mwandishi mwandamizi aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha, marehemu Adolf Balingilaki, ambao unasema kwamba:
“Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu watakudharau.

KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri, dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze kwani ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.

Karibu tuelimishane na kusaidia pale unapojua niko tayari kujifunza toka kwako; naamini ili niweze kujua zaidi natakiwa kujifunza kupitia wenzangu.  

Karibuni sana tusonge mbele kwa ushindi.

Lusako Mwakiluma

Friday, July 18, 2014

AINA 4 YA WATU KATIKA ULIMWENGU WA MAFANIKIO


Ni imani yangu kuwa, si wote wanafahamu kwa undani aina nne za watu katika ulimwengu wa mafanikio, jambo ambalo naamini linachangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya hawa wafanikiwe kimaisha na wengine wasifanikiwe kabisa.
Kwa kufahamu hilo, nimeona ni vyema nikaandika makala haya kuhusu aina za watu katika ulimwengu wa mafanikio ili kuamsha akili za watu katika kukabiliana na changamoto nyingi za kimaisha.

Kwenye ulimwengu wa mafanikio binadamu wamegawanyika katika makundi manne ambayo ni WATENDA USAHIHI, WANAORIDHIKA, WANAOTAKA KUPENDWA NA WASHINDI. Naomba tufuatane katika kuangalia kwa undani aina hizi za watu ili kuanzia leo kila mtu afahamu yupo kundi gani.

WATENDA USAHIHI: Ni watu ambao katika maisha yao huwa hawataki kukosea au kuonekana wayafanyayo si sahihi. Watu wa aina hii huwa ni wagumu sana kufanya jambo ambalo akili zao hazihakiki kuwa litamalizika kwa mafanikio.
Kikwazo kikubwa kwa watu wa aina hii mara nyingi ni kusitasita katika kuamua. Ni watu wa kuogopa macho ya watu hasa suala la kushindwa kutimiza malengo linapowajia akilini. Kinachowaogopesha zaidi watu wa kundi hili ni kuabika mbele za watu jambo fulani likiwaharibikia.

WANAORIDHIKA:
Kundi jingine la watu katika ulimwengu wa mafanikio ni wale wanaoridhishwa na hali zao na kwamba hawahitaji mabadiliko ya aina yoyote kwenye maisha yao. “Ndugu yangu, hali hii tumeizoea, mwaka wa nne.” Wamezoea maisha magumu.
Hata hivyo, wapo wanaozoea kazi na majukumu yao ya kila siku kiasi kwamba hawataki kubadilika, hawapendi kuongezeka zaidi ya hapo walipo. Utakuta uwezo wa mfanyakazi alioanza nao miaka 7 iliyopita ni huohuo mpaka leo. Wafanyakazi wengine wanaweza kuajiriwa nyuma yake wakajitahidi kusoma, kujifunza kazi na kupanda vyeo na kumwacha mridhikaji yuko palepale. Kundi la wanaoridhika.

WANAOTAKA KUPENDWA: Kuna watu katika maisha yao wanataka kumfurahisha kila mtu kwa lengo la kuvuta upendo wa wanadamu wenzao. Utakuta maisha yao yote ni kuwatumikia wengine kutoa fedha za maendeleo kwa kumsaidia huyu na yule kwa malipo ya kupendwa na jamii.
Ni wazi kuwa watu wanaoishi katika kundi hili hawawezi kufanikiwa kwa sababu kipato chao kingi hukitumia katika kuwafanya watu wengine wafurahi na si kusukuma mbele maisha yao ya kila siku.

WASHINDI: Kundi la mwisho la watu ni wale ambao katika maisha yao ya kila siku hupenda kufika kwenye kilele cha mambo yote wanayofanya. Hutamani kufanikiwa zaidi na zaidi, hawakubali jambo liwashinde, kila walichokusudia kukifanya huhakikisha kwamba wanakabiliana na changamoto zote na mwisho wa safari kupata ushindi.

Baada ya kuangalia hayo, ni vema kujiuliza; Je ni sahihi kutokuwa makini katika mambo yako ama kuridhika na mafanikio uliyoyapata? Inawezekana kweli mtu akaacha kusaidia wenzake kwa hofu ya kuwa katika kundi la tatu? Jibu ni hili:
Ni vema mambo matatu  ya mwanzo yakaongozwa na la nne yaani USHINDI. Kwa maana hiyo kila mmoja wetu lazima awe mtu ambaye anatamani sana kufanikiwa katika maisha yake ya kila siku.  Watu wote wakiwa na nia hii wataweza kuyapita makundi mengine matatu kwa uangalizi mkubwa.

Hawatakubali wawe makini wasifikie malengo, hawataacha kujaribu bahati kwenye mambo ambayo akili zinaona ni magumu, hawataridhishwa na mafanikio au hali walizonazo na hawatakubali kutumika kama kuwafurahisha watu bali kila kitu watafanya kwa kiasi kwa lengo la kufika katika mafanikio sahihi.
Haya dunia yako, chaguo ni lako. 

Asante kwa kusoma mada zangu karibuni sana tuelimilishane!!

Thursday, July 3, 2014

ANGALIA FURSA KWA NAMNA YA KIPEKEE (SEEING WHAT OTHERS DON'T)

Leo nakuletea mada ambayo inaweza kutusaidia kubadilisha mfumo wetu wa kufikiri na namna ambavyo tunaweza kuangalia vitu kwa namna ya pekee.

Tanzania ni moja ya nchi ambayo imebahatika kuwa na rasilimali nyingi sana za aina tofauti tofauti katika kila nyanja lakini sisi watanzania tumekuwa tukiendelea kubaki katika hali ya kutojitambua na pindi wageni wanapokuja ndani ya nchi wanatumia rasilimali tulizo nazo na wanapata upenyo wa kufanikiwa huku tukiendela kuwaona kama wachawi. Kumbuka unapokiona wewe kitu hakifai na kukidharau au kutokuwa na mtazamo sahihi ndipo inakuwa kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi.

Katika eneo hili tumejaribu kuangalia mambo machache ambayo yanaweza kukusaidia kuweza kujitambua kuweza kusonga mbele katika maisha yao bila woga na kujidharau huku ukijua faida yake katika siku zijazo. Ukiwa kama ndugu, jamaa, rafiki unaweza ukaamua kufanya mabadiliko yako mwenyewe bila kushurutishwa wala kulazimishwa na mtu.

1.Social Yardstick(VIpimo vya Kijamii)
Muda mwingine kwenye maisha yetu tumeshindwa kuzitumia fursa ambazo tunazo sababu tumetumia jamii kama sehemu ya kipimo chetu cha kuendesha mambo na vitu vyetu. Mfano Utasikia "Yaani mtoto wa fulani hakufanikiwa na alikuwa na akili sana wewe ndio utafanikiwa?.Unaposikia hivyo mara nyingi watoto wetu wamedumaa na hata akili zetu zimedumaa tumeshindwa kujua watu wengine ni wengine na sisi ni sisi. Jaribu wewe mwenyewe usitumie mtu mwingine kama kipimo chako cha maendeleo."USIISHI KWA KUIGA HAUTAFIKA MBALI”

Kuitumia jamii kama kipimo chako cha kuendesha vitu ni makosa jaribu kutumia uwezo wako na nguvu zako ili kuweza kupiga hatua kwenye nyanja nyingi za maisha yako binafsi hata ya familia yako. Mfano…"Mara nyingi familia nyingi zimetumia watoto wengine kama kipimo cha malezi kwa watoto wa familia zao na sio wao kama wao wanaweza kulea na kuwakuza watoto wao, uzuri au ubaya wa mtoto hautokani kuwa mtoto wa jirani yako ni mzuri au mbaya".

 2.Comparison(Kujilinganisha)
Hili limekuwa miongoni mwa matatizo makubwa kwa tumetumia watu wengine kama sehemu ya kipimo cha mafanikio ya fulani ingawa si vibaya kujua mwingine anafanya nini. Unapotumia muda mwingi kujilinganisha na mwingine unapoteza uwezo wako halisi wa kufanya vitu katika uwanda mpana wa maisha yako. Kumbuka kila mtu ana maono na ndoto zake kwenye maisha yake unapojaribu kuwa kama yeye unaishi maisha yake wakati wewe sio yeye. Jifunze kuishi maisha bila kujilinganisha linganisha na wengine maisha ni kujaribu kutumia fursa zilizopo.Kumbuka unaweza ukafanya zaidi kuliko mtu unayejilinganisha naye kwa kufanya zaidi na vizuri sana, hii inakuletea hali ya kujiamini wakati wote.  Na kujifahamu kuwa wewe ni halisi.

Unaweza ukajikuta unafanya vitu chini ya kiwango kumbe uwezo unao na huo uwezo unaweza ukawa ni mkubwa zaidi ya hapo.  Usiogope kuthubutu na kujaribu na usiangalie nani anasema nini walioshindwa ndio waliofanikiwa.  Jifunze katika kushindwa.  Na walioshindwa wana maneno mengi ebu badilika na tumia kushindwa kwako kuwa ushindi kamili.

“Fikiria Barak Obama, Hillary Clinton, Bill Gates, Les Brown, Napolean Hill, Ben Carson na    wengine wengi waliofanikiwa wangejilinganisha wangefika pale walipo. 

Simama kwa nafasi yako na fanya kwa uwezo na nguvu zako zote bila hofu.  Kumbuka riziki ya mbwa iko miguuni, akilala hawezi kupata anachotaka na wewe jiangalie umetoka wapi na unaenda wapi endelea mbele ukiifuata hatima yako  kwani wakati ni mali na kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.

 "ANGALIA FURSA KWA NAMNA YA KIPEKEE”

Na: Lusako Mwakiluma