Naomba tutafakari zaidi na zaidi kuhusu maisha ya familia kwani
uhai wa familia ni uhai wa Kanisa na taifa zima la Mungu. Maisha ya familia ni
zawadi kubwa ambayo Mungu ametujalia tangu pale alipoumba ulimwengu kwani yeye
aliona kuwa “si vema huyu mtu awe peke yake, nitamfanyizia msaidizi wa kufanana
naye” (Mwanzo 2:18).
Hapa tunaona hekima ya Mungu ya kumuumba mume na mke na
kuwaambia kuwa “Kwa hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na
mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Mwanzo 2:24). Tunaishi katika
ulimwengu wenye changamoto nyingi ambazo tusipokuwa macho zinaweza kuhatarisha
ule umoja kati ya mume na mke, umoja ambao Mwenyezi Mungu anatuambia kuwa “Mwanadamu asiutenganishe”.
Tunapoendelea kutafakari kuhusu maisha ya familia na changamoto
zake katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia, leo hii ningependa
tutafari pamoja kuhusu tatizo la kuvunjika kwa Agano la ndoa kati ya Mume na
Mke katika jamii zetu. Jambo hili linaonekana kama kitu cha kawaida katika
ulimwengu wetu wa leo.
Kadiri ya Mafundisho ya Kanisa ambayo msingi wake ni Maandiko Matakatifu kama tulivyoona, Agano la Ndoa Takatifu ambalo linatambulika na Kanisa kama Sakramenti linaweza kutenganishwa na Mungu pekee pale kinapotekea kifo cha mwenzi mmoja wapo. Hivyo basi, pale wenzi wawili(Mume na Mke) wanaposema kuwa wanapendana kwa dhati, upendo huo sio upendo wa majaribio bali ni upendo unaowaalika wapenzi hao wawili kila mmoja kujitoa kwa mwenzake mzima mzima bila kujibakisha.
Hii hali ya kijotoa kwa mwingine ni sadaka kubwa katika maisha kwani wapenzi hawa wanakubali kupokeana kama walivyo katika raha na taabu, maana yake wanakubali kusaidiana kuubeba msalaba wa maisha katika mazingira yoyote kwa lengo la kuupata utakatifu.
Na Lusako Mwakiluma
No comments:
Post a Comment