Tuesday, July 7, 2015

UMUHIMU WA ELIMU YA NAFSI NA UFAHAMU


Huwezi hata kidogo kutenganisha maisha ya mwanadamu na elimu ya saikolojia, elimu ambayo katika ulimwengu wa sasa wengi wanaisikia  lakini wachache wanaotambua umuhimu wake, achilia mbali maana ya neno lenyewe.  Mimi nimeona nikupe maarifa haya baada ya kuona mwenyewe inanisaidia na pia kupitia Asasi ya WEZESHA TRUST FUND imewasaidia wengi na watu wamepona magonjwa, wameshinda majaribu na leo hii wanafurahia kuifahamu naomba na wewe uwe mmoja wao ambaye ukisoma mada hii utajua jinsi ya kuenenda.

Injinia wa  kwanza aliyeipa nguvu elimu hiii ni  mwanasaikolojia  wa Kijerumani, Wilhelm Wundt ambaye alifungua maabara  na kutibu watu kwa kisaikolojia, zoezi ambalo  lilileta matokeo  ya kushangaza ulimwengu mzima.  Huo ulikuwa ni mwaka 1879.

Saikolojia ni ‘mtoto’ wa neno la Kigiriki lijulikanalo kama ‘psyche’ au akili na roho jina ambalo baadae  lilikuzwa  na kufahamika  kama ‘Psychology’, tafsiri  ikiwa Elimu ya Nafsi  na Ufahamu.  Katika nchi zilizoendelea somo hili linapewa nafasi  ya juu katika maisha ya binadamu kutokana na  umuhimu wake.  Wanasema wataalamu kuwa, kuishi  bila kujua tabia za vitu na watu pia na  ukuaji wake na kujifunza mabadiliko yake ni sawa na kutembea katika kamba ndogo ya maisha salama.  Unatakiwa ufahamu watu, wanyama, ndege na vitu vinavyokuzunguka ili uweze kushinda majaribu au changamoto zinazokuzunguka.

Saikolojia ni somo ambalo kila kukicha binadamu anatakiwa kufundishwa kwa vile hakuna anachoweza kukifanya kisiguse  akili na  nafsi  yake.   Inashauriwa  kwamba ni lazima mtu ajifahamu  mwenyewe pia awafahamu wengine, mazingira anayoishi na mabadiliko yake wakati wote, tunaishi katika nyakati na majira na unatakiwa ufahamu kila jambo linakupata linaanzia ndani yako mwenyewe.  Unaweza ukalitengeneza bila kufahamu au mazingira yakalitengeneza ukijua kabla haikusumbui.

Maswali ya msingi yenye kumuongoza  binadamu  vizuri katika  maisha yake ni  haya.  Mimi ni nani, kwa nini niko hivi?  Wale ni  watu ni akina nani?  Kwanini wako  vile na tunapaswa  kuwa vipi baadaye, pamoja na kujiuliza kwa nini vitu vipo kama vilivyo.
Imebainika kwamba, mvutano  wa nguvu za dunia na za binadamu huongezeka mara dufu kwa mtu ambaye hajui Saikolojia ya Maisha.   Dunia kama sayari na mwanadamu kama kiumbe kila  mmoja amekuwa akitengeneza  nguvu zake za kumuwezesha  kuwepo, huku uzalishaji  wa nguvu hizo kwa upande mmoja ukikinzana vikali na mwingine, hata hivyo madhara makubwa  yamekuwa yakiwakuta  binadamu ambao ndani yao kuna uhai ambao ni sisi wenyewe.

Hata hivyo, uchunguzi  unaonyesha kwamba ufahamu, nafsi na akili umebaki kuwa kinga muhimu ya mwanadamu katika  ulimwengu huu ambao umekuwa unabadilika  mara kwa mara.  Hatari iliyokuwepo siku hizi ni  hasa kwa ulimwengu huu wa tatu ni ukosefu wa elimu hii muhimu, jambao ambalo limewafanya watu  wenyewe kwa wenyewe kuzalishiana nguvu za kuangamizana  na kuiacha dunia  ikishinda mara zote na watu kupoteza maisha pasipo muda wao kufika au kuharibikiwa na mambo yao wakidhani ni hali ya kawaida.

Inahuzunisha  pia kufahamu  kwamba mbali  na binadamu kushindana na  mabadiliko  ya ulimwengu na nguvu zake, wengi wao  wamekuwa  wakipambana  na nguvu zao wenyewe ndani ya  miili yao bila kujijua, kiasi cha kupoteza maisha.

Tafiti za wanasaikolojia zinaonesha kwamba asilimia kubwa ya matatizo yanayomwangalia  binadamu yanatokana  na yeye mwenyewe  au jamaa zake, huku ushahidi  ukionesha  kuwa hata magonjwa ya kutisha kama moyo, kansa kisukari, vidonda vya tumbo na mengineyo yanachangiwa na  kiasi kikubwa na mawazo ya mtu mwenyewe.  Magonjwa mengi hayapo ila watu wanayazalisha katika nafsi zao mwishowe yanaenda kutokea kwa hofu zao na woga waliokuwa nao.

Karibu katika Blog yetu uendelee kupata mambo mengine mengi muhimu ili uweze kujikwamua na hali ya kushindwa na kuweza kushinda katika kila eneo la maisha yako na kupona magonjwa yako yanayokusumbua kwa muda mrefu.


Na: Lusako Mwakiluma Maheri

Wednesday, May 20, 2015

JINSI YA KUFANIKIWA NA KUWA TAJIRI


Jinsi ya kupata mafanikio: Ufunguo wa utajiri na kufanikiwa ebu soma haya kwa makini:
Utajiri na mafanikio sio  karama ya watu wachache. Wote tunao uwezo wa  kuupata kwa kiasi tunachotaka katika maisha yetu.  Jifunze siri ya nguvu za kupata mafanikio, utajiri kwa haraka katika maisha yako.

Kwa nini watu wengi wanataka kufanikiwa, utajiri na kwenda mbele katika maisha na wengi wetu hatuna hivyo vitu.

Kwanini?
Sababu kubwa ni kwamba tunafikiria sana hasi au tunafikiria vitu vibaya.   Kutokana na kufikiria kinyume na vibaya tunaenda kupoteza muda mwingi kwa kujiwekea vipingamizi wenyewe vya mafanikio.

Tunapoteza muda mwingi kwenye vile tunavyovikosa na kuja kuwa wafungwa  katika mafikirio yetu. Ili tuweze kupata  mafanikio katika maisha inabidi tubadilishe mtazamo wetu na tabia ambayo tumeishaizoea.

Ondoa hali ya hasi na karibisha kukua katika mafanikio yako. 
Unatakiwa uondoe kabisa hali ya hasi katika fikra zako zote na mawazo yako yote angalia mbele na jiweke vizuri katika kila unachokifanya na kwa mtu wowote unayekutana naye.  Tunajifunza kutoa shukrani kidogo  ili tuweze kuona  kile ambacho tunakosa  na kile ambacho tutakiongeza au fursa zikoje?

Unatakiwa uwe makini sana  na kila kitu kimoja, mtu au  sehemu ambayo ni muhimu katika kupata fursa  kwa hiyo utaenda kupata  kukua kimafanikio, fursa na hata  kupata utajiri unaoutaka katika maisha yako.

Usiruhusu mawazo hasi  yakuaribie mtazamo wako au nafasi ya kupata fursa, mafanikio na furaha, tengeneza tabia ya kuangalia vizuri katika kila kitu hivyo basi  usiangalie chini ambako hakuna fursa.  Kama utaona hakuna kitu, jifunze jinsi ya kuona kuwa mtazamo ni sehemu ndogo ya ukweli na upige picha kwa kupitia umuhimu na uwezekano wa kufanya kitu.

Njia za kuweza kupata  mafanikio na utajiri
·         Panga mipango: Fahamu kwamba  kama unataka kufanikiwa.  Panga mipango yako. Jiangalie mwenyewe  kama mtu  ambaye unao uwezo wa kufikia malengo yako.

·         Jiangalia tokea ndani: Fuata nafsi yako inasema nini wakati wote  kukuhakikishia msaada  kwa kuona mbele hasa wakati  ule ambao unahitaji msaada.  Nafsi ni ngumu kuelezea ila kila mmoja anajua na anao uzoefu wa mawazo makubwa kuhusiana na kitu fulani na wakati wote unaweza ukajitenga na kuumia.

·         Piga picha: Pata mafanikio na utajiri  kwa kupiga picha mipango yako na fanyia mazoezi  fahamu zako kama vile umeshapata hayo mafanikio.

·         Matendo: Usifikirie kitu utakachofanya ili uweze kufikia malengo yako ila  fanya ili ufikie malengo yako.  Kama unajua unataka kubadilisha maisha yako  na mtazamo wako, fanya hivyo.  Hata kama unaona ni ngumu kwa kutoa sababu nyingi, jipe ujasiri na endelea mbele kwa kufanya mwenyewe.

·         Jifunze kutokana na uzoefu: Jifunze kutafakari na kuangalia kwa undani maisha yako, uzoefu wako, na mahusiano yako.  Jifunze kutokana na  makosa ya awali na elewa  kwanini unabadilisha  mafikirio yako na utakubalije vikwazo  katika mafikirio na imani.   Acha hali ya hasi  na kutumia nguvu ndogo inayokuzunguka kwa sababu wakati mwingine vinakusimamisha na  kukupa mzigo mkubwa.

·         Fuata shauku yako:- Mwisho napenda nikwambie kitu muhimu sana  kwa sababu ya kufanya kile unachokipenda sana, hakuna sababu ya wewe kushindwa au kuogopa kuendelea kufanya ili ufanikiwe.

Wengi wetu wanaenda na maisha wakiwa vipofu, wamekata tamaa na hawana furaha, je unayo mawasiliano ya ndani na wewe mwenyewe na yabadilishe kuwa yenye manufaa kwa mtazamo wako na utakuwa umejihakikishia  kupata mafanikio unayoyataka katika maisha yako.

Ni juu yako kuamua sasa!!

Thursday, April 2, 2015

JINSI YA KUJITAMBUA MWENYEWE


Kama binadamu unatakiwa ujitambue  ili uweze kwenda na wakati au kufanya yale ambayo yanatakiwa  kufanyika  na yale ambayo hayatakiwi kufanyika usiyafanye.
Kuna mambo  ya msingi ya kuyafanya  ili uweze kufikiria  vizuri  wakati wote.  Na kila mtu atakayekuona  atajua huyu mtu amejitambua na amejua  umuhimu wake katika jamii inayomzunguka kwani utajikubali  wakati wote  na kuwaheshimu wengine.
Moja
Fikiri vizuri (jenga mfumo wa kufikiri vizuri); mfumo huu uwe endelevu; siyo usubiri upate tatizo ndiyo uanze kufikiri  vizuri  (usiwe kama zima moto).  Hii itakusaidia  kuanza kupanda mbegu njema kwenye mawazo yako ya kina ili maisha yako ya baadaye  yawe mazuri; yatoe mbegu nzuri/njema.

Mbili
Rudisha mawazo yako nyuma, jenga picha  yako ya utotoni.  Chagua taswira moja wakati ulipokuwa mtoto jione kimwili, kimavazi na mazingira ulipokuwa (nyumbani /shuleni au popote).  Kisha rudi kwako sasa hivi ukiwa mtu mzima; jione kama ulivyo sasa hivi ukiwa unamtazama huyo mtoto ambaye  umemjengea taswira; mtoto ambaye pia ni wewe.  Mtazame  na zungumza  naye, mwambie ulidanganywa kwamba ni mbaya; huna akili, huna thamani, huwezi, hufai nk; na wewe  uliamini kwa sababu ulikuwa mtoto.  Lakini sasa umekuwa mkubwa; fahamu ukweli halisi kwamba wewe ni mzuri, una akili unaweza na una thamani  sawa na wengine; unaweza na unafaa.  Rudia zoezi hili mara kwa mara; kila wakati hakikisha  unachagua  eneo ambalo  uliambiwa  huwezi; Futa  imani zote mbaya kwenye mawazo yako ya kina.

Tatu
Ni ile ya kufanya zoezi la kurudia rudia maneno pamoja na kujenga taswira  mfano: kila wakati  jiambie ninaweza; ninafaa; nina thamani, najiamini.  Imani ni muhimu sana wakati unajimbia maneno hayo.

Nne
Hapa utaenda kutumia mshumaa, uwashe mshumaa; uweke mbele yako juu ya meza au stuli au sehemu yoyote.  Angalia ile sehemu  ya mshumaa inayowaka moto (siyo mshumaa wote) kwa muda wa dakika 10, 30 au zaidi.  Baada ya hapo fumba macho yako yote ili uuone ule moto wa mshumaa  kwa kutumia macho yako ya akili (yaani jicho la tatu).  Utaenda kuona moto huo ukiwa wa kijani, bluu, njano au mweupe.  Baada ya kuuona, anza kuchoma zile tabia  au mambo  yanayokukera au kuwakera  wengine mfano: Choyo, wivu, uzinzi, dharau, zichome  moja baada ya nyingine.  Wakati unazichoma utaona moto wa mshumaa ukiongezeka  ukubwa au utaona moshi.  Fanya zoezi hili mara kwa mara. Baada ya muda utashangaa kuona tabia au mambo hayo yamekwisha na tabia hizo umeziacha kabisa.

Tano
Ni ile hali ya kutumia kioo, simama jitazame kwenye kioo ikiwezekana kila siku asubuhi na jioni.  Tafuta zile kasoro ambazo uliambiwa  na jiambie kwamba huna.  Kama uliambiwa wewe ni mbaya; Basi jiambie wewe ni mzuri, huku ukijiangalia bila kujiogopa kwenye kioo.  Lakini kama uliambiwa huwezi, jiambie naweza sana.  Pia jikubaai kama ulivyo na jiambie umekamilika, una thamani na unastahili.

Sita
Ni ile hali ya kupata nafasi ya kuyapa mawazo yako ya kawaida  baada ya kupewa nafasi ya muda  hatimaye yatachukuliwa mawazo yako ya kina, mambo haya  mapya  yataua au kukausha ile miche/miti iliyoota  kwenye mawazo  yako ya kina; miti hii ni ile ya mambo ambayo yanakukera au kuwakera wengine. Kwa ile ambayo imeshazaa matunda haiwezi kukauka kwani umeshaanza kuvuna kitu ambacho nidyo maisha unayoishi hivi sasa.  Njia hizo zote tano ni za mzunguko.  Hii ya sita  ni ya njia ya mkato kwani unaenda moja kwa moja  kwenye mawazo yako ya kina na kuyaambia yale unayoyahitaji ambayo ni kinyume na yanayokukera.

Nguvu ya uumbaji kitaswira  na kujipa nguvu
(i)                 Kumbuka: Imani – hisia- matokeo
(ii)               Ondoa mipango ya zamani kwenye  mawazo ya kina ndiyo sababu ya msingi ya kukwama kwani nyuma ni historia na inatia uchungu ukiifikiria.

Kuna aina tatu ya uumbaji  kitaswira: sauti, kuona na hisia.
(iv)             Kila mmoja ana aina yenye kutawala kwake awe anajua au la.  Kuna wengine  wanatawaliwa  na aina mbili.  Katika matumizi ya uumbaji kitaswira, tunaanza na aina yetu, baadaye tunajifunza nyingine.

(v)               Ili kujua aina yako, jaribu kufikiria unachohitaji sasa hivi ili uone.  Mwanzoni unaweza kusikia  sauti inayokuambia hutaweza au ni mzaha ufanyao.  Unatakiwa ufanye  mazoezi  mengi ili uweze kujenga uwezo wako ulionao au uliopotea.

(vi)             Mawazo yako ndiyo  yenye  kukufanya/kukuwezesha ujenge uumbaji kitaswira.  Unachokiona kila siku ni matokeo ya kilicho  mawazoni kila siku. Hivyo, bila kujua huwa tunaumba yale tusiyoyataka maishani.  Uumbaji  kitaswira unawakilisha utunzaji wa mbegu (mawazo) kutegemea  ni mbegu gani tumepanda.

(vii)           Makosa  yajitokeza sana; usiweke  nguvu  kwenye kukosa, kwenye usichotaka na kwenye usichonacho.   Mfano: kama umepanga kwenye chumba  kimoja na unataka kujenga nyumba yako, usijiambie nimechoka  kukaa kwenye  haka kakibanda au maisha ya kupanga yamenichosha.  Sema lazima niambie nyumbani kwangu yaani nyumba niliyojenga mwenyewe.

(viii)         Unapokuwa  kwenye uumbaji  kitaswira, hisi au  ona kama vile jambo limeshakuwa  tayari – piga picha ya utayari wa jambo lako.

(ix)                                                                                   Jinsi ya kufanya (hatua);
(i)                 Tafuta mahali tulivu
(ii)               Tuliza mawazo yako
(iii)             Weka nguvu zako  za mawazo  katika jambo  unalolitaka

(x)                Simamia kufikiria vizuri wakati wote utakaokuwanao na utashangaa kuona matokeo mazuri na kwa muda mfupi sana.

Na: Lusako Mwakiluma

Wednesday, March 25, 2015

JINSI YA KUKUTANA NA MITIHANI BILA HOFU


Hii ni hali ya kisaikolojia.  Angalia kupata zaidi kutoka na neno linalokwenda.  Uangalie  mitihani  kama mtu anayekuja kukudai deni lako na anataka wewe umlipe.   Hapo  utaongozwa na hali ya wakati huo.  Wewe ni mdeni unayedaiwa.  Wewe ni mhusika.   Kuwa mhusika mkuu au mdaiwa inakupa ujasiri.   Kuwa jasiri 

Kuwa jasiri maana yake unatakiwa kukabili hali hii bila hofu.  Mfano; Unatakiwa  sasa ulipe deni na mdeni nae  hataki kuondoka mpaka umpe pesa yake, kama ni wewe unafanyaje? Unatakiwa uwe mtulivu kisha umpe mikakati ya jinsi ya kulilipa deni aidha umechelewa  kuna sababu itabidi umpe za kumfanya aridhike na kuweza kukuongezea muda wa kuweza kulipa kama ulivyomuahidi.  Usimkimbie  wala usikatae  kuongea naye  utapoteza ujasiri wa kukabiliana na mitihani yako.

Muhammad Ali, alikuwa bingwa wa mchezo wa saikolojia.  Aliingiza hofu ndani ya moyo wake kabla ya kupigana kwa njia ya kutengeneza ushindi kabla ya pambano.   Ali alikuwa  anatafakari  ushindi wakati wote.  Alikuwa  anapigana  kisaikolojia  na mwishoni aliingia ndani ya uwanja kama mshindi siku ya pambano kwani aliweza kumsoma  anayepambana  naye kupitia  michezo ya nyuma.

Wengi wameshindwa  kumpiga Muhammad Ali na walikuwa wanapigwa kabla hata mchezo haujaanza.

Geogre Foreman alikuwa na uzito mkubwa katika siku zake za mapigano.  Watu wachache waliweza kupigwa kwenye mzunguko wa  kwanza tu walipopigana nae.  Foreman alikuwa na uzito mkubwa sana kuliko mahasimu wake.  Kabla ya mchezo ambao sitausahau na George Foreman kule Zaire.  Ali alizungumza  na dunia jinsi alivyojiandaa kupigana na huyo hasimu wake.  Alijihakikishia ushindi na alikubali  yote kwamba anaenda kufanya kitu cha tofauti.

Ndiyo, unaweza kufikiria kitu gani kilitokea  siku hiyo ya mpambano.  Kwa wakati  ule kengele  ilipopigwa kwa mara ya kwanza, George  Foreman  alikuwa ni mtu aliyepigwa tayari.  Ali alijitahidi kumtoa nje kwa mazungoko wa kwanza tu.

Jiandae na wewe kwa mtihani kama Ali alivyojiandaa kupigana na  George Foreman  na hakuwa na hofu ya kupigana naye (Work Hard, Work Smart then Trust God).

Nawasilisha.
Lusako Mwakiluma


Thursday, February 12, 2015

NJIA KUMI NA MOJA(11) ZA KUJIHAMASISHA MWENYEWE


1.      Kuwa na furaha
Amua kuwa na furaha sasa  kwa chochote  unachokifanya fanyia mchezo wa jambo hili mara zote. Fanya maamuzi  haya yatakuhamasisha wewe mwenyewe.  Jipe furaha mwenyewe shughulika na vile unavyovipenda na furaha itakuja na pia kaa na wale unaowapenda na furaha yako itakuwa ya kwako wakati wote.  

2.      Tenda kwa tabia  yako
Jinsi  unavyotenda ndivyo  utakavyokuwa mfano unatakuwa  Dr  au Prof. anza kutenda  kama Dr na Prof wanavyofanya  kazi soma sana fahamu vitu kwa kina na sio juu juu tu ingia ndani  au unataka kuwa  mwalimu fanya kama mwalimu anavyofanya  usijaribu jitahidi  ufanye kama unavyotaka bila hofu.  Itakuletea hamasa ya kuweza kuwa kama unavyotaka kwa muda mfupi sana.

3.      Kaa peke yako
Usifanye kitu, pumua na jiangalie mwenyewe kama vile mchunguzaji kwa muda kisha kwa muda utaanza  kujisikia mabadiliko mazuri yanaanza kuja kwako kwa ndani.  Mabadiliko yanaanzia ndani yako jihamasishe na utaona mabadiliko taratibu.

4.      Safisha
Safisha  mazingira yako  yanayokuzunguka kwani mazingira  ni mapana na ndiyo yanayotuvuta kwenda huku na huku na yakiwa sio masafi yatakufanya usiwe kama unavyotaka hivyo  yakiwa masafi utajisikia  vizuri mfano:Unataka kuwa mwalimu basi tengeneza  mazingira  kama walimu wanayoyatumia.

5.Tumia  kupiga picha yako
Tumia nguvu zako  kuangalia maisha yanayokuhamasisha na hamasa yako itafuata.  Mfano; unataka kujenga  nyumba piga picha ya nyumba inayoitaka halafu hii itakuletea  nawe kujihamasisha kujenga ya kwako kwa mfano ule.  Kwani picha hiyo unaweza ukaiweka katika kioo chako au chumbani mwako mahali ambapo utaenda kuiona kwa muda unaoutaka na hii itakuinua sana kuweza kupata hamasa kubwa sana.

6. Ondoa hali ya wengine wanavyokuangalia
Jipe ruhusa sasa ya kutojali watu wanasemaje kuhusu wewe.  Badala yake  weka utulivu wako na kuwafanya wengine  wajisikie vizuri wao wenyewe.   Maisha yatabadilika kama utafanya hivi wakati wote na kwa hiari yako mwenyewe bila kulazimishwa na mtu yeyote.  Unaweza kubadilisha tabia yako bila kushinikizwa na mtu yeyote katika maisha yako.  Na wale wanaokuangalia watashangaa sana kwani hawakujua kama uko kazini katika kuwafanya wajisikie vizuri wao wenyewe na kukuacha ukifanya yako bila kikwazo chochote.

7. Jiulize maswali mwenyewe 
Maswali utakayojiuliza mwenyewe yataenda kuamsha ufahamu wako:-
1.         Kitu gani kizuri kwenye maisha yako – majibu yake yatakufanya  ujue unatoka     wapi na kwenda wapi na kukitafuta hicho kizuri na kukifanyia kazi.
2.         Kitu gani  ambacho bado hakijafanyika kwako namaanisha ambacho bado haujakifanya?  - Angalia nini bado haujakifanya na kwanini haujakifanya changamoto ya kutaka kujua itakupelekea uwe jasiri wa kufanya kwa muda uliobakia hata kama muda umekwenda sana utashangaa kuona miujiza inatendeka kwa muda mfupi sana.

8. Yaangalie  tena matatizo yako
Kila suluhisho lina matatizo.  Anza kuangalia  fursa  zinazotengenezwa na matatizo yaliyopo:-
Mfano: Wauza maji walianza kuuza maji baada ya tatizo la maji kuwa kubwa katika sehemu zinazowazunguka.
Hospitali zilijengwa baada ya kuona idadi ya wagonjwa ni kubwa na hakuna mahali pa kupata matibabu wala dawa.

9. Chukua hatua za mtoto
Jaribu kuvunja vunja kile unachokitaka kwa kukipanga hatua kwa hatua.  Kisha nenda hatua moja moja kama mtoto anavyofuata hatua zake kuanzia kuzaliwa mpaka anaenda kutembea.  Hii itakusaidia sana kuweza kukamilisha mipango yako yote uliyojiwekea  na haitakuwia vigumu kuanza kwa sababu unaanza na hatua ndogo ndogo.  Utaenda kutambaa, utasimama, kisha utaanza kutembea na mwishowe kukimbia kwa hatua ndefu ndefu.

10. Pata wazo jipya
Chukua  kalamu yako na andika  malengo yako  au kitu unachotaka kufanya kwenye maisha yako.  Andika juu ya  karatasi ya kwanza na uweke orodha 1 mpaka 20.   Andika mawazo 20 kwa kujihakikishia kuyafanya. Fanya kwa kadri unavyoweza na kupenda huku ukijihamasisha mwenyewe.   Anzia namba moja mpaka ishirini kwa uhakika wa kuangalia na muda unavyokwenda ili uweze kujua ni kwa muda gani umekamilisha jambo lako ili uweze kuendelea mbele na jambo lingine.

11. Fanya kitu hata kikiwa kibaya kwanza
Usisubirie mpaka ufanye vizuri  jaribu kuanza na kukutana na changamoto ndogo na kubwa.  Cheka kwa jinsi unafurahi hata kama umekosea hali hii itakusababishia  kwenda kubadilika  nawe ndio utabadilika kwa hali unayoitaka.  Usiogope kukosea kwani wote waliokosea au kushindwa ndiyo leo hii wamefanikiwa sana.  Usiogope watu watasemaje kuhusu kushindwa kwako.  Simama katika nafasi yako na fanya kwa usahihi na Mungu atakusaidia kwani neno usiogope lina nguvu sana katika kutenda.
Na: Lusako Mwakiluma
Mhamasishaji & Mhelimishaji






Wednesday, October 22, 2014

KUFANYA YASIYOWEZEKANA LAZIMA UWE NA NDOTO YA KUTOWEZEKANA



Ukitaka kufanya kitu kisichowezekana lazima uwe na ndoto ya kutowezekana ndipo utakapoona hili ni tatizo na lazima litatuliwe. Tunapoenda kuangalia rekodi ya matukio au shughuli za mwaka kwa mwaka au katika rekodi ya historia kila mafanikio yametokana na hali ya kutowezekana kwanza na kulikuwa na hali ya changamoto ya ugumu wa mafanikio kabla na wengi walisema haiwezekani.  Hapo ndipo ushindi unapatikana katika hali ya kutowezekana.  Ebu mwangalie Alexander Braham Bell mfumbuzi wa kwanza wa kutengeneza simu au mawasiliano au Martin Luther King Jr au Susan B. Anthony ambaye alihakikisha wanawake wanapewa kibali cha kupiga kura au Nelson Mandela wa Afrika Kusini aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini baada ya kutoka jela na hakuna aliyejua kama atatoka kwa muda wote aliofungwa ni miaka mingi lakini iliwezekana na mtazamo wake au ndoto yake ilikuja kuwa ya kweli.

Wote hao waliendelea mbele huku wakijua haiwezekani huku wakiwa na shauku ndani ya mioyo yao.  Ukitaka kupata kitu muhimu lazima uwe na kushindwa kwanza.  Kitu usichowahi kukifanya hata siku moja lazima uchechemee kwanza kabla haujafikia malengo. Hata mtoto anapozaliwa lazima apitie kukaa, kutambaa, kusimama kisha kutembea hawezi kuzaliwa leo na kuanza kutembea ikitokea hivyo basi itakuwa ni historia lazima iandikwe magazeti na kwenye radio itangazwe.  “Ukitaka kupata kile ambacho haujawahi kukipata ni lazima ufanye kile kitu ambacho haujawahi kukifanya” alisema Rais Obama wakati hajawa Rais akiwa kwenye maisha ya kawaida sana na binti yake mmoja akiwa amemkumbatia pembeni ya gari bovu mitaa ya uswahilini kabisa.  Lakini leo hii unamuona akiwa Rais na maisha bora yenye kutamanisha.  Hajakurupuka Rais Obamaule alijipanga mpaka kufika alipofika na leo hii anaheshimika ametimiza ndoto yake. Kumbuka mwenye maono hafi mpaka ameyatimiza.  Ukimuona mtu mwenye maono amekufa bila kutimiza basi ujue hakuwa dhahiri katika ndoto zake alikuwa mzungumzaji na sio mtendaji wa anachokisema na akishindwa yeye basi hata mtoto wake anaweza kutimiza kama waliwahi kuongea na mwenye maono.
  

 

 

Thursday, September 4, 2014

CHANGAMOTO ZA MAISHA



 Kwa sababu tumeumbwa tofauti, wako walioumbwa kushughulika na mambo ya wenzao tu muda wote wanaangalia fulani kafanya nini na kafanikiwa au kashindwa kwa kiasi gani.  Mwisho wa siku ukiwaangalia watu hawa utajikuta unashindwa kufikia malengo yako na kukwama njiani katika safari yako ya maisha.  Ndugu yangu simama katika nafasi yako na usiwaangalie walioshindwa, walioshindwa wana maneno mengi sana.  Na ukiwafuata watakupotezea dira kabisa.  Amini kile unachokifanya na amini kwamba kitafanikiwa kwa asilimia mia moja pamoja na hali zilizopo usirudi nyuma Mungu ni mwema kwetu siku zote na yeye anaangalia mwisho wako sio mwanzo wako. 

 Kuna watu wameumizwa, kuna watu wameachwa, kuna watu wamekimbiwa na kuna watu wamefiwa na kukataliwa na kuonekana si kitu kwenye jamii zao zinazowazunguka.  Nakuomba ndugu yangu usifikirie kujiua au kususa kwa ajili ya maisha yako simama ukijipa moyo kwamba wewe sio wa kwanza unayepitia haya mama yangu nimpendaye sana Maya Angelou mwandishi wa vitabu na misemo yake mizuri alisema katika mahojiano yake na Oprah Winfrey “kwamba kila unachopitia amini sio wa kwanza kukipitia wapo waliopitia unayopitia tafuta njia mbadala na kisha endelea mbele” nakwambia muda sio wetu hata kwa kuuza maji ya mia mia utatoka tu.  Usikae chini na kukata tamaa utapoteza dira yako.

Hayo yaliyopita chukulia kama changamoto na hao waliokuacha na kukumbia wachukulie kama ngazi ya kupandia kuelekea kwenye mafanikio yako na yachukulie ya jana kama historia ya kuja kuwashuhudia watu waliokuwa na hali kama hizo kwa baadae.  Amina tu na songa mbele kwani adui ni ngazi ya kupandia na unaombwa kila siku kumpenda adui yako, jiulize je., huyu adui yangu akifa huyu nani atakuja kunipigia makofi wakati naenda kufanikiwa na kuwashuhudia wengine nilikotoka?.  Kuwa na roho ya unyenyekevu na ya msamaha kwa yeyote anayekwenda kinyume na wewe kwani hakuna barabara ndefu bila kona na hakuna yaliyo marefu bila kuwa na ncha.  Kumbuka kwa wale wakristo Danieli, Meshack na Abelnego waliwekwa kwenye tanuru na hawakuungua kwa sababu ya imani ya Mungu wao waliyemwamwini kwanini usiwe wewe ule moto ni changamoto kama hizi ninazokuhadithia hapa.  Naamini kuna watu wanaenda kupokea miujiza yao ya mafanikio kupitia changamoto hizi za maisha nasema maisha ni rahisi kama unayapatia na ni magumu kama unapoteza muda kuangalia tatizo badala la suluhisho la tatizo lako.  Jiulize Bill Gates, Obama, Hillary Clinton wao wamezaliwa na nani na wananguvu gani za kukushinda wewe ambaye una masaa hayo hayo na nguvu kama zao.  Inuka twende mbele tusipoteze muda wala saa.

Nakutakia usomaji mwema wa mada zangu na Mungu atakuinua kwa namna ya tofauti mpendwa. 
Karibu sana
Lusako Mwakiluma